Shirika la Habari la Hawza, - Je, mfumo wa Uimamu uliisha kwa kumalizika kwa kipindi cha "ghaibatu-sughra" na kuanza kwa "ghaibatu-kubra", na kwamba baada ya kudhihiri kwa Imam Mahdi (as) ndipo mfumo huu utaanzishwa tena, au ni kwamba mfumo wa Uimamu unaendelea mfululizo bila kukatika?
Mfumo wa Uimamu ni mfumo wa kimungu, hauna kukatika, hauna kipindi cha mapumziko, na upo katika kila zama. Kuanzia zama za Mtume Mtukufu (saw) hadi sasa, mfumo huu umeanzishwa na umeendelea kuwepo, na kadiri dunia itakavyokuwepo, mfumo huu utaendelea kuwepo. Kama alivyosema Amirul-Mu’minin (as):
«لَا تَخْلُو الْأَرْضُ مِنْ قائِم لِلهِ بِحُجَّهٍ؛ إِمَّا ظَاهِراً مَشْهُوراً، أَوْ خَائِفاً مَغْمُوراً، لِئَلَّا تَبْطُلَ حُجَجُ اللهِ وَبَیِّناتُهُ.»
“Ardhi haitakosa mwenye kusimama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa hoja; aidha akiwa dhahiri na maarufu, au akiwa na khofu na amejificha, ili hoja za Mwenyezi Mungu na bayana Zake zisibatilike.” (Nahjul Balagha, Hikma ya 147)
Kwa hiyo, ni lazima kwa kila mtu kuutambua mfumo wa Uimamu, kuuamini, na kuufuata. Na katika kila zama na kila mahali, watu wanapaswa kufuata mfumo huu tu.
Kila mtu ni lazima afanye wazi na aweke bayana kwamba katika maisha yake na katika kila hali na jambo la maisha, anafuata mfumo upi na anatii serikali ipi. Ni lazima aonyeshe wazi kama amekubali kufuata utawala wa Mwenyezi Mungu au wa taghuti; kama ni muumini wa Mwenyezi Mungu au wa taghuti.
Kwa masikitiko makubwa, Waislamu wengi hawatilii maanani suala hili muhimu sana, hawaifahamu vizuri maana ya "wilayah", na wameghafilika na umuhimu wa kipengele hiki, ambacho ni utiifu. Na hata wale walio waumini wa kweli na waaminifu, hujitosheleza tu kwa kutekeleza wajibu wa baadhi ya faradhi na kuacha haramu.
Kwa mujibu wa madhehebu ya Kishia, ambapo mfumo wa Uimamu ni wa kudumu na endelevu, kufuata serikali halali ya Kisharia ni miongoni mwa wajibu wa kimsingi katika kila hali.
Utawala ni wa Mwenyezi Mungu pekee:
إِنِ الْحُکْمُ إِلَّا لِلّٰهِ
“Hukumu ni ya Mwenyezi Mungu tu.”
Ni Yeye tu anayepaswa kuabudiwa na kutiiwa, na ni lazima utiifu huo uwe wa dhati kwa ajili Yake:
أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِیَّاهُ مُخْلِصِینَ لَهُ الدِّینَ
“Ameamrisha kuwa msiabudu ila Yeye tu, hali ya kuwa ni wenye kuitakasa kwake yeye dini.”
Dini ya sawa na iliyonyooka ni hii:
ذَلِکَ الدِّینُ الْقَیِّمُ
“Hiyo ndiyo dini iliyonyooka.” (Yusuf: 40)
Mfumo wa Uimamu ni sawa na serikali ya Mwenyezi Mungu; kuufuata ni kusalim amri kwenye hukumu ya Mungu, kuishi katika dola ya Mwenyezi Mungu, na kutoamini katika utawala usio wa Mwenyezi Mungu. Hivyo basi, hakuna tofauti – iwe katika zama ambazo Maimamu (as) walikuwa dhahiri lakini wakiwa wametengwa na madaraka ya wazi, au katika zama za (ghaibatu-kubra) ambapo Imam (as) yupo mafichoni – kila Mwislamu lazima afuate mfumo wa Uimamu.
Na kwa kuwa kuamini katika mfumo wa Uimamu ni tawi la imani katika Tawhidi na katika utawala wa Mwenyezi Mungu na mamlaka ya haki, basi mtu yeyote atakayekufa bila ya kumtambua Imam wa zama zake, amekufa kifo cha kijahili: kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw):
«مَنْ مَاتَ وَلَمْ یَعْرِفْ إِمَامَ زَمَانِهِ مَاتَ میْتَهً جَاهِلِیَّهً.»
“Atakayekufa bila ya kumtambua Imam wa zama zake, amekufa kifo cha kijahili.” (Bihār al-Anwār, juz. 32, uk. 321)
Na kwa kuwa kumtii kiongozi asiyekuwa wa haki ni aina ya shirki ya kiitikadi na kimatendo, Imam Sadiq (as) amesema katika hadithi:
«لَا دِینَ لِمَنْ دَانَ اللهَ بِوِلایَة إِمَامٍ جَائِرٍ لَیْسَ مِنَ اللهِ.»
“Hana dini mtu anayemwabudu Mwenyezi Mungu kwa uongozi wa Imamu dhalimu asiye toka kwa Mwenyezi Mungu.” (al-Kāfī, juz. 1, uk. 375)
Kutokana na hadithi hizi inafahamika kuwa mfumo wa Uimamu si wa muda au wa wakati maalum tu, bali ni wa kudumu na wa milele. Haukuwahi kusitishwa, wala hautasitishwa.
Utafiti huu unaendelea...
Imenukuliwa kutoka katika kitabu “Majibu kwa Maswali Kumi Kuhusu Uimamu” kilichoandikwa na Ayatollah Safi Golpaygani – huku ikifanyiwa mabadiliko kiasi
Maoni yako